Sunday, November 25, 2012

Ufumbuzi wa kisaikolojia wa tatizo la ugumba

Ni ukweli usiopingika kuwa ndoa nyingi zimepoteza furaha kutokana na watoto kukoseka miongoni mwa wanandoa. Wanawake na wanaume wamejikuta wakiangukia katika mikono ya matapeli wanaojiita waganga na kufanyiwa mambo mengi ya ajabu, ikiwa ni pamoja na kufanya mapenzi na mizuka au na watu ambao hawakuwatarajia ili tu waweze kupata watoto. Hakuna ubaya wa kutafuta tiba ya ugonjwa endapo upo, lakini kutafuta tiba ya ugonjwa ambao haupo ni kuchosha mwili na matokeo yake huwa ni mabaya zaidi. Uchunguzi uliohusisha matatibu kutoka hospitali na vituo vingi vya afya unaonesha kuwa wagumba wengi wanaosaka tiba hospitalini wamebainika kutokuwa na matatizo ya kibaiolojia. Ninaposema kibaiolojia nina maana kwamba wanandoa wengi wagumba wamekutwa wakiwa na uhai katika viungo vyao vya uzazi. Katika ulimwengu wa leo idadi ya watu wanaokosa watoto bila kuwa na sababu ya msingi inatajwa kuwa ni kubwa na kila siku wasichana na wavulana wanaingia katika chumba hiki cha huzuni isiyojulikana chanzo chake. Kukosa uzazi bila sababu ni tatizo ambalo limekuwa likizisumbua akili za wahitaji watoto wengi na mwisho kuwagotesha katika mawazo ya kurogwa na sababu kubwa ikiwa ni kutojulikana kwa chanzo cha wazi cha kutokuzaa kwao. Ukweli pekee ambao nimekusudia kuuzungumza leo kuhusiana na wasiokuwa na matatizo ya uzazi kutokuzaa ni ule ambao umeshawekewa misingi na watafiti walioandika taarifa yao katika jarida la Minerva Ginecologica la nchini Italia kwamba uchovu unaoletwa na mawazo ndiyo unaochangia kwa kiasi kikubwa watu wasipate watoto licha ya kwamba kibaiolojia hawana matatizo. Tafiti za hivi karibuni zimebaini kuwa, wanawake wengi wenye viungo salama lakini hawazai, wana kiasi kikubwa cha homoni ya Cortisol inayoletwa na uchovu. Kwa mujibu wa utafiti huo aina hii ya homoni ndiyo inayosimamisha mchakato wa uzalishaji mayai kwa wanawake wakimbia riadha. Hivyo basi uwiano huu wa kasoro za ukuzaji mayai kati ya wakimbia riadha na wanawake wagumba unaweka usawa baina ya uchovu mkubwa wa mazoezi ya viungo na ule uchovu unaotokana na msongo wa mawazo ya ugumba. Uchovu wa kihisia huweza kumfanya mwanaume au mwanake asiweze kuzaa kabisa katika maisha yake. Hii ina maana kuwa watu wanaotingwa zaidi na mawazo ya kukosa fedha, migogoro katika ndoa zao na kujaribu mara kadhaa kupata watoto bila mafanikio wana uwezekano mkubwa wa kutokuzaa hata kama maumbile yao yataonekana kitabibu hayana kasoro. Imebainika kuwa watu wengi hujisogeza wenyewe katika nguvu ya kukosa mtoto kutokana na ukubwa wa kiu yao ya kupata mtoto, huku wakilazimisha kimawazo mchakato wa kubeba au kubebesha mimba kwa wakati ulipangwa na malengo yao. Mkazo huu wa mawazo huwakumba hasa wanandoa na wapenzi ambao wanatamaa ya kupita kiasi ya kupata mtoto katika uhusiano wao. Hawa hujiweka katika uzalishaji mkubwa wa homoni ya Cortisol ambayo huchipuka kwa kasi kutokana na msukumo wa kiu kubwa na ya haraka ya kukumbatia mwana. Kutokana na ukubwa wa tatizo hili la msongo wa mawazo, imebainika kuwa wagumba wengi wasiokuwa na kasoro katika viungo vya uzazi wanaweza kupona au kupata watoto bila hata kupewa tiba ya miti shamba au vidonge. Tiba yake kubwa iliyobainishwa ni kupatiwa nasaha zitakazowaondolea mawazo tasa, wasiwasi na kutojiamini. Ukweli wa tiba hii ya ushauri imethibitishwa hivi karibuni na kituo kimoja nchini Marekani kinachojishughulisha na utafiti wa kuzalisha watoto, ambapo majibu yake yalichapishwa katika majarida na mitandao mbalimbali. Kwa mujibu wa taarifa ya kituo hicho asilimia 75 ya wanawake waliokosa watoto ambao walifika kituoni hapo na kupewa ushauri walifanikiwa kuzaa baada tu ya kuhudhuria kliniki na kupewa ushauri uliowatoa katika msongo wa mawazo. Nasaha ambazo zimekuwa zikitolewa na wataalamu hao si ngumu, bali ni zile zilizojaa maneno yenye kugeuza fikra hasi zenye kuondoa kiu kali ya kupata watoto kwa utashi na nyakati zilizopangwa na wahusika. Pia wagumba hufundishwa namna ya kuepuka migogoro ya kimapenzi na kutoumizwa kupita kiasi na kejeli za watu kuhusiana na kutozaa kwao, huku wakijengewa imani kuwa kuzaa ni suala linalowezekana kwao, hivyo kuwafanya watupilie mbali hofu na mawazo kuwa wao ni wagumba. Lakini pamoja na nchi zilizoendelea kuwa na vituo vya kutolea nasaha kwa waathirika, bado wanasaikolojia wanakiri kwamba mtu mwenyewe anaweza kujiepusha na uchovu unaoletwa na mawazo kwa kurahisisha tatizo lake kutoka kutowezekana na kuwa linawezekana kutatuliwa. Akili ya mtu ndiyo inayopima na kuongoza utambubuzi wa ukubwa wa tatizo na si kwamba kuna matatizo makubwa na madogo kama watu wanavyofikiria. Kwa maana hiyo ili mtu ambaye amejiwekea ukuta wa kutozaa kwa msongo wa mawazo yake kama nilivyosema aweze kuzaa lazima aondoe mawazo ya kwamba yeye ni mtu asiye zaa, kwani hakuna mtu wala vipimo vilivyompa majibu ya kwamba ni mgumba. Jambo jingine la kufanya ni kupuuza maneno ya kukatisha tamaa toka kwa watu wengine. Hii ina maana kuwa lawama zozote toka kwa mume/ mke au wanafamili zinazohukumu kosa la mtu kutokuza lazima zipuuzwe na zisipewe nafasi ya kutia simanzi moyoni. Sambamba na hilo kuna suala la wanawake kuzingatia kalenda zao kwa kujichunguza na kubaini muda muafaka wa kukutana kimwili na mwanaume ili kupata matokeo mazuri ya utungishaji mimba. Kwa mantiki hii kuna wanandoa wengi wameshindwa kupata mtoto kwa kutozingatia siku zenye uwezekano wa kupata mimba ambazi ni siku ya 11 hadi ya 16 tangu siku ya kumaliza hedhi. Lakini kwa kuwa kuna suala la utumiaji wa dawa za uzazi wa mpango ni budi wahusiaka kusimamisha matumizi yake pindi mtoto anapohitajika ndani ya ndoa. Hata hivyo kuna umuhimu wa kutumia mitindo ya kuvuta kizazi nyakati za kufanya mapenzi, ili kuzipa msukumo wa haraka mbegu kunasa kwenye mfuko wa uzazi. Sambamba na hilo wanaume wanatakiwa kuepuka ufanyaji holela wa mapezni ili kuzifanya mbegu zikomae na wakati wa tendo kuvuta hisia kali ili kuongeza msukumo wa manii kutoka kwenye uume kwenda kwenye uke. Na jambo la mwisho katika mchakato wa kupata mtoto ni lishe bora miongoni mwa wanandoa. Lazima miili iwe na nguvu za kutosha kusimamia uzalishaji wa mbegu bora. Inashauriwa wanaume waepukane na uvaaji wa nguo za ndani za kubana ambazo zinatajwa kuongeza joto kwenye kiwanda cha kuzalisha mbengu na hivyo kuzidhoofisha.

No comments:

Post a Comment