Sunday, November 25, 2012

VYANZO VITANO VYA BAHATI MBAYA

“Alikuwa anavuka barabara, lakini kwa bahati mbaya akagongwa na gari.” “Nimemaliza masomo yangu mwaka jana, lakini kwa bahati mbaya nikafeli.” Kwa bahati mbaya biashara yangu ilisambaratika.” “Kwa bahati mbaya alifukuzwa kazi.” Imetokea kwa bahati mbaya” Nimebata bahati mbaya Mume wangu hanifai hata kidogo.” “Kwa bahati mbaya alijifungua mtoto aliyekufa” Hizi ni baadhi kauli za baadhi ya watu ambao ni wafuasi wakubwa wa kitu kinachoitwa bahati mbaya katika maisha yetu ya kila siku. Hebu tujifunze vyanzo vya bahati mbaya na namna ya kuepukana nayo, ili tusijikute kila siku tunalaumu kupatwa na bahati mbaya kumbe makosa ni yetu na kwamba hatukuwa makini katika kuishi kwetu. UZEMBE WA KUFIKIRI Watu wengi wanaoamini kuwepo kwa matukio ya bahati mbaya katika maisha wanaelezwa na wataalamu kuwa na kasoro katika upeo wa kufikiri vyanzo vya mambo. Inasemwa na watafiti wengi kuwa matukio mabaya yaliyopata kuripotiwa ulimwenguni ni matokeo ya uzembe wa kufikiri na kuamua. Kwa maana hivyo inashauriwa kuwa mtu anayetaka kuepukana na bahati mbaya lazima awe hai katika fikra, hasa upataji wa jibu la mapema juu ya nini kitatokea katika kutenda kwake. Inampasa mvuka barabara kwa mfano, ajiuliuze matokeo ya kuvuka kwake na apate majibu chanya na hasi na ahakiki matokeo hasi ambayo kwa kawaida ndiyo yenye madhara. Vivyo hivyo kwa dereva anayeendesha chombo cha moto, msichana anayetaka kuolewa, mfanyabiashara, mfanyakazi, anayefanya mapenzi, anayesoma, wote kwa ujumla wao lazima wawe na majibu ya kwa nini wanataka/ wanafanya hayo, kisha wajadili akilini matokeo mabaya ambayo yapo na kuyatafutie njia ya kuepukana nayo. KUTOTUMIA UWEZO WOTE Mwanadamu natajwa kuwa na uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo kuliko wengi wao wanavyodhani. Uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha kuwa asilimia 70 ya watu ulimwenguni, hasa wale wa dunia ya tatu wanaishi chini ya uwezo na vipaji walivyonavyona. Kwa kuzingatia hilo wahanga wengi wa bahati mbaya ni wale ambao hawatumii uwezo wao wote au zaidi ya nusu ya vipaji vyao katika kupambana na matokeo mabaya. Wanafunzi wengi hawasomi kwa uwezo wao wote, wataalamu, wanasiasa, viongozi, watendaji hawatumii uwezo wao wote kufanya kazi na majukumu waliyonayo, matokeo yake wanalipua kazi na baadaye kuleta matokeo mabaya kisha kuyapa jina la BAHATI MBAYA. Inasemwa kuwa kila mahali palipo na janga msingi wa kwanza kutazamwa kwa watu wenye uelewa ni UZEMBE na kutotumika kwa uwezo halisi wa wahusika katika kukinga matokeo mabaya. KUAMINI VIASHIRIA VYA KUSHINDWA Kuna watu ambao hupatwa na matokeo ya bahati mbaya baada ya kuamini viashiria vya kushindwa na kuacha kujizatiti katika nguvu za ushindi. Kwa mfano timu ya mpira inaweza kufungwa magoli 3 kipindi cha kwanza, matokeo hayo yakiaminiwa na wachezaji yanaweza kunyonya nguvu ya ushindani na kuikaribisha bahati mbaya, kumbe wangepuuza viashiria hivyo vya kushindwa mapema wakaongeza nguvu wangeweza kurudisha na pengine kushinda mchezo. Vivyo hivyo, tunapokuwa tunafanya jambo fulani, kuna viashiria vinaweza kujitokeza kututia hofu kwamba tutashindwa, tunashauriwa kutokata tamaa. Kama wewe ni muuguzi umemuona mgonjwa wako anashindwa kupumua usipunguze harakati za kumtibu kwa kuamini viashiria kwamba anakufa muda mfupi ujao, badala yake zidisha juhudi za kumuokoa. Mfanyabiasha pia ukiona biashara inayumba usikate tamaa, ongeza bidii kwa kufanya hivyo utakuwa unapambana na bahati mbaya na kwa mujibu wa wanasaikolojia utakuwa umenyonya nguvu za mabaya na hivyo kutokukupata. KUYUMBA KATIKA MAAMUZI Kuna watu ambao kwa hakika kabisa wanaweza kuwa wamefikiri vema, wametumia uwezo wao wote, hawakuamini viashiria, lakini wakajikuta wanapatwa na bahati mbaya kwa kuyumba katika maamuzi, hasa wakati wa kuhitimisha jambo fulani. Kwa mfano mtu anaweza kuwa ametafuta mchumba, akamhakiki kama nilivyosema, lakini likatokea neno la umbea fulani likamyumbisha na akajikuta amemwacha mchumba wake na kuchukua mwingine ambaye hakumhakiki katika fikra. Inashauri kwamba mtu asiyumbe katika maamuzi sahihi aliyoyathibitisha. KUMBUKUMBU MBAYA Katika maisha yetu kuna watu wengi ambao wanasogeza bahati mbaya kwa kujaza kumbukumbu mbaya za matukio hasi kwenye akili zao. Wapo mahodari wa kukumbuka mahali zilipotokea ajali za magari, yaani wakifika hapo tu mioyo inakwenda mbio. Kuna wanaokumbuka rafiki zao waliokufa wakati wanajifungua na wengine wana historia za nani alipatwa na mabaya baada ya kufanya jambo fulani na wengine wanawafahamu kwa majina waliokufa bila kuzaa, yote hayo ni kujitia hofu tupu. Kuishi na wingi wa kumbukumbu mbaya ni kosa kubwa kwani hutengeneza uzembe wa mwili ambao huleta matokeo mabaya bila mhusika kujijua. Ndiyo maana unaweza kukuta ajali nyingi hutokea zaidi eneo moja kutokana na madereva wapitao hapo kujaza kumbukumbu mbaya ambazo huwaondolea umakini. Hivyo kama tunataka kuepukana na bahati mbaya ni vema tukaondoa kumbukumbu mbaya zinazotia hofu na hata kama tutakumbuka iwe kwa ajili ya kuongeza umakini na isiwe kwa kupata woga wa kuvuka salama eneo au tukio hilo.

No comments:

Post a Comment