Sunday, November 25, 2012

HATA WEWE UNAWEZA KUFANIKIWA

MAFANIKIO hutokana na jitihada katika maisha tunayoyaishi. Watu wengi wanaopenda kufanikiwa mara zote hutafuta mbinu mbalimbali ili kutimiza ndoto zao. Hivyo basi unatakiwa kuota ndoto ya mafanikio yenye malengo makubwa. Binafsi ninaamini katika malengo hayo kuwa kuna mafanikio endapo utamaanisha. Wakati mtu anapoanza kuwa na malengo makubwa, anaanza kwa kufikiri jinsi Mungu alivyomwezesha katika jambo hata kufikia hatua na kufanikiwa. Ndoto hiyo ya mafanikio haina gharama, ni jinsi ya unavyoweza kujipangia muda na ratiba zako. Kumbuka ukiwa na malengo ya mafanikio haitakugharimu chochote. Unaweza ukawa na malengo ya kuanzisha mradi mkubwa pasipokuwa na fedha, inabakia kuwa ni ndoto tu. Mungu alianza kuumba dunia ikiwa haina kitu. Tunaweza kuwa na malengo makubwa ya mafanikio katika maisha yetu, haijalishi ni ya aina gani. Unapokuwa na ndoto hiyo ya kutaka kufanikiwa, kamwe usiruhusu moyo wako kuvunjika au kuwa katika hali ya kukata tamaa na wasiwasi. Kwani hali hiyo itakudhoofisha na kukufanya usisonge mbele, bali urudi nyuma. Unapohitaji jambo kubwa kutokea katika maisha yako unatakiwa kuwa na maono mapya. Kumbuka hata wewe unaweza ukawa na maono makubwa ya ajabu. Haijalishi ni mtu wa aina gani, umetoka wapi au umepatwa na jambo gani, katika hali uliyonayo unaweza kuwa na maono mapya. Kumbuka malengo makubwa hayawi kwa watu waliofanikiwa, bali ni kwa wale wanaotaka kufanikiwa. Vyovyote uwazavyo, ndoto inainua na kuweka kitu kipya katika maisha yetu, inatutengeneza na kutusogeza mbele, inatuwezesha kufikia malengo makubwa tofauti na ilivyokuwa awali. Inatuwezesha kufanya kitu kikubwa ambacho hatujawahi kukifanya tena kabla ya hapo. Je, wataka kuwa fulani? Kusimama nje ya kusanyiko kubwa? Kukumbukwa? Hali hiyo inakuwepo ndani ya mioyo yetu inayodunda na kutaka kupata siri ya mafanikio. Tunataka kuwa fulani. Inawezekana, ndiyo inawezekana. Mungu ametoa kwa kila mtu uwezo na vipaji mbalimbali. Wakati Mungu anakuumba alikupa kipaji na akasema kama utatumia kipaji ulichonacho atakiongeza, na kama hutatumia kipaji ulichonacho utakipoteza. Kukitumia kipaji chako au kukiachia ni juu yako wewe! Dunia yetu imejaa vipaji vingi na uwezo ambao hautumiwi. Unatakiwa kulima kwa bidii, na kupalilia ili upate mavuno bora. Tumia kipaji chako kabla hujakipoteza. Unaweza kudhani kuwa hauna kipaji chochote, si kweli, labda inawezekana haujagundua kipaji chako. Inawezekana umekiweka kipaji chako kabatini. Amini kuwa kila mmoja anacho kipaji chake alichopewa na Mungu. Waweza kutumia kipaji ulichonacho au kukipoteza. Maisha yetu yamejengwa katika kanuni hiyo. Kuna mifano mingi ya kupoteza au kupata, hiyo ni kanuni ya kawaida. Chukua hatua ambazo zitaifanya ndoto yako kuwa kweli. Ota ndoto yenye thamani katika maisha yako. Kama hauna malengo, haitawezekana matarajio yako kutimia. Ndoto inaanza unapokuwa na wazo. Kumbuka watu huvutiwa na wenye maono makubwa. Chagua maono yenye matarajio. Baadhi ya watu wanapoteza muda wao kwa kuwa na malengo ambayo hayatawasaidia. Mfano, kuna kijana katika miaka iliyopita alisaidiwa kupewa ushauri baada ya kupoteza muda wake mwingi akifikiria ni jinsi gani ataweza kumpata mke wa jirani yake na kumfanya awe wake. Ndoto yake hiyo haikuwa ya thamani ya muda mrefu. Wakati wazo linapokujia katika ufahamu wako, iulize nafsi yako maswali matatu. Je, jambo hilo litampendeza Mungu? Litawasaidia watu wanaoteseka? Kwa maneno mengine litakuwa msaada kwa watu? Litaleta mafanikio mazuri kwako? Kama jibu lako ni ndiyo katika maswali yote, utakuwa na maono yenye mafanikio. Unapoamua kufanya jambo fulani, usijiulize ulize kuwa hii ni njia nyepesi ya mafanikio? Au ni njia rahisi? Inaweza kuwa na usalama? Haitakuwa na vikwazo? Hakuna utakachoshindwa utakapofanya bidii. Hakuna mwenye nguvu ya kuua ndoto yako, isipokuwa wewe mwenyewe. Panga mipango vizuri kwa kuwa huwezi kujenga bila ramani. Huwezi kufanikiwa matarajio yako pasipokuwa na malengo makubwa. Ninamfahamu mtu aliyekuwa na maono makubwa lakini yalikuwa hayafiki mbali. Ni kwa sababu alikuwa hana ramani ya maono yake. Hakikisha unatimiza ndoto uliyojiwekea. Malengo yako hayawezi kufanikiwa kama hujajitoa kufanya hivyo. Ili kufanikiwa katika mipango yako unahitaji juhudi na kufanya kazi kwa bidii ili upate mafanikio. Amua pa kuanzia. Fanya uamuzi sahihi. Panga muda wa kuanza. Usitafute sababu ya kuacha kufanya malengo yako kwa muda ulioupanga. Katika dunia yetu kuna watu wengi wenye mipango mingi lakini hawaifanikishi. Jiondoe katika kundi hilo. Fanya kitu. Andika barua, piga simu. Anza hatua ya mafanikio. Jiamini waweza kutimiza ndoto zako. Wakati unajaribu kupata mafanikio utaona kuwa ni kipindi kigumu kwako. Hali ya kukata tamaa inakuwepo katika moyo wako, ikisema jiondoe katika hatua ambayo unataka kuianza ya kupata mafanikio katika maisha yako, kataa. Kama unakutana na kipindi cha majaribio katika biashara, ndoa, mambo yako binafsi, kwenye wingi wa watu au hali ya maisha uliyoizoea na uko tayari kukabiliana nayo, songa mbele usikate tamaa. Unachofanya ni kujaribu kupata mafanikio, tena mafanikio makubwa. Katika kila mafanikio unayoyapata, kuna gharama ya kulipa. Kumbuka huwezi kupata ushindi bila kulipa gharama.

No comments:

Post a Comment