Sunday, November 25, 2012
Mtazamo wa wanaume kuhusu wanawake wa kuoa
Zama tunazoishi sasa zimetambulishwa kuwa kuolewa ni jambo la bahati miongoni mwa wasichana wengi. Wanaume kama ‘vipanga’ wawindao tayari wameshajua kuwa wasichana wengi wana kiu ya kutaka kuolewa.
Kwa maana hiyo wanaitumia hamu hiyo kama chambo cha kuwanasa wanawake na kuwatumia kama wastarehesha miili na hatimaye kuwaacha solemba.
Wanaume wengi siku hizi hawapapasi njia ya kujipatia mpenzi msichana wa kutosheleza tamaa zao kwa vile kauli hii inatosha: “Mimi naitwa Kauta (siyo jina sahihi) nimevutiwa sana na wewe, nataka uwe mchumba wangu.”
Laghai hii kwa mujibu wa uchunguzi wangu haina mipaka, inatumika mashuleni, maofisini na kwenye idara mbalimbali za kazi na wasichana wengi wamejikwaa kwenye mapenzi kwa ahadi za kuolewa.
Kwa wanaume siku hizi idadi ya wachumba haijalishi, wanaweza kuwa tisa kumi au zaidi ilimradi kuna kukata kiu kwa kujikusanyia warembo wengi. Maana siyo ajabu kumsikia mwanaume amewavalisha pete za uchumba wanawake zaidi ya watatu na kuwatumia kwa miaka mingi.
Karibu asilimia tisini ya wasichana vigori wametumbukia katika uhusiano wa kimapenzi kwa kudanganywa kuwa ni wachumba na hivyo kulegeza msimamo wa kutunza heshima yao kwa woga wa kupoteza bahati ya kuolewa. Kibaya zaidi wazazi nao wanachangia kuwaingiza mabinti zao kwenye mtego huu.
Jambo baya zaidi ni kwamba asilimia zaidi ya 80 ya wasichana huachwa njia panda na wengine kuambulia mimba na magonjwa toka kwa hao waliowaita wachumba. Nimesikia na kuona wanawake wengi waliokuwa na wachumba wakiachwa na waliowapa heshima ya “mchumba wangu.”
Nina ushahidi wa kesi nyingi za wasichana kuchezewa na kupotezewa muda mwingi na kujikuta kwenye majuto ya “Naumia sana, nimekuwa naye kwa miaka sita lakini leo kaniacha na kuoa mwanamke mwingine.”
Kwa mtazamo wa ndani bado kuna upofu wa elimu ya kimapenzi katika jamii yetu hasa kwa wasichana. Umbumbu huu unatokana na ukweli kwamba mapenzi yamekuwa ni kitu cha aibu ndani ya familia nyingi, si baba wala mama anayeona thamani ya kumfundisha mwanae utambuzi wa masuala ya kimapenzi, ili kiwepo kizazi kinachoweza kutofautisha mapenzi ya kweli na ya uongo.
Ukitazama makundi yawasichana wa leo utagundua kuwa wengi kati yao wamejiweka katika fungu la wanawake wa kustarehesha na si wa kuoa. Hii inatokana na ukweli kwamba hawajafundishwa namna gani wanaweza kuwa wanawake wa kuolewa kwenye jamii.
Wote tunafahamu kuwa wasichana wengi siku hizi wameingia katika mkumbo mbaya wa kuvaa mavazi ya nusu uchi, bila kujua sababu za uvaaji huo na namna gani wanavyotazamwa na wanaume
Sote tunafahamu kuwa yapo madai ya kwenda na wakati kwa wadau wa ‘vichupi na vimini.’ Lakini wasichana hao hao wanashindwa kufahamu kuwa wanaume hawajabadilika katika mahitaji ya kutafuta wanawake wenye tabia njema kuwa sehemu ya mahitaji yao ya kuoa.
Nimebaini katika uchunguzi wangu kuwa wanaume wanavutiwa zaidi na wasichana wenye kuvaa vichupi, si kwa maana ya kuwaoa bali kustarehe nao ki mwili na kujitwalia sifa: “Ha, jamaa kapita na demu mkali ile mbaya.”
Pamoja na hilo, ukweli unabaki kuwa mtazamo wa wanaume juu ya wasichana wa kuoa na wa kustarehesha unataofautiana. Wanaume wengi wa leo kwa mujibu wa utafiti wangu wanapenda zaidi kuoa wanawake watulivu, wenye kujiheshimu, kujiamini na wasiokuwa tegemezi.
Lakini linapokuja suala la sterehe wanaume hao hao hupenda zaidi wanawake wasiojiheshimu, wanaosita sita kuingia gesti, walio tayari kukwaruzana na wazazi wao kwa kurudi nyumbani bila muda maalum na hodari wa mavazi ya aibu.
Uchunguzi unaonesha kuwa wanaume ambao hukutana na wanawake watulivu huku wakiwa na nia ya kustarehe nao, huwabadilisha tabia taratibu ili waendane na matakwa yao na wanapogeuza nia kwa maana ya kutaka wanauwake wa kuoa huwatelekeza hao na kurudi kwenye kundi tulivu.na kuoa huko.
“SIWEZI KUMUOA DEMU HUYO KWANI HAJATULIA, NILIKUWA NAZUGA NAYE TU” Huo ndiyo unakuwa mwisho wa uchumba hewa na msichana anakuwa ameshachezewa kwa miaka mingi na kuachwa na sifa mbaya miongoni mwa jamii.
Ushauri wangu kwa wasichana wote ni kuwa makini na mtego huu wa wanaume kwa kushikilia utulivu na heshima ambayo ni msingi imara si wa maisha ya ndoa tu bali hata ya jamii iliyostaarabika. Lakini pia mtaji sahihi wa kuolewa kwa dunia ya leo ni uwezo wa kujitegemea, uimara wa kusimamia maamuzi sahihi yanayohusu maisha na ujenzi wa mapenzi yenye malengo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment