Sunday, November 25, 2012
Jinsi mtu anavyoweza kupata furaha ya kweli maishani
Karibu kila mtu anatafuta furaha kwa njia mbali mbali anazoona zinafaa. Wapo wanaoamini kuwa wakipata wake/waume, kazi, utajiri, wakijenga nyumba, wakipandishwa cheo na kufaulu mitihani watafurahi sana.
Lakini tafiti zinaonesha kuwa asilimia 87 ya wanaohangaika kutafuta hayo wanayodhani yatawafurahisha huwa hawafurahi sawa na matarajio yao ya awali. Wataalamu wanakubaliana kuwepo kwa furaha katika siku za mwanzo za kutimia kwa malengo ya watu, lakini kiwango cha furaha kimebainika kupungua kadili mtu anavyozidi kuishi ndani ya kile alichokitamani au alichodhani akikipata kitamfurahisha.
Ukubwa wa furaha ya siku ya kuchumbiwa, kununua gari, kuhamia katika nyumba mpya, kupandishwa cheo, kuongezwa mshahara, kuolewa au kuoa, hushuka kila siku na hivyo kumfanya mtu afikia hatua ya kuona alichokipata si kitu cha kufurahisha sana na hivyo kuingiwa na mawazo ya kutafuta vitu vingine ambavyo atavipa nafasi kubwa ya kumfurahisha.
Unaposoma haya jaribu kukumbuka moja kati ya vitu ulivyovihangaikia na hatimaye kuvipata, siku hiyo ulikuwa na furaha ya kiwango gani ukilinganisha na sasa?
Bila shaka unatambua kuwa ulivyofurahi siku ulipoolewa ni tofauti na unavyofurahi leo, ingawa ndoa uliyoitafuta ni ile ile na mwanaume uliyenaye ni yule yule, tena inawezekana mlipooana mlikuwa na maisha ya chini lakini leo mmefanikiwa isipokuwa furaha imepungua.
Hapo kuna jambo la kujiuliza kwa nini wengi wetu tunashindwa kupata furaha ya kweli na kubaki kila siku ni watu wa kuhangaika kutafuta hiki na kile cha kutufurahisha. Mara nyingi kwa uzembe wa kuwaza anachokuwa nacho mtu si bora kuliko kile anachotafuta. Mwanamke mzuri daima hawi mkeo bali ni wa jirani, ndiyo maana wengi hufumaniwa na kwa mshangao wanawake ambao hufumwa nao huwa si wazuri ukilinganisha na walionao.
Kama nilivyoeleza awali kwamba tuna kila sababu ya kujifunza namna ya kutafuta na kupata furaha ya kweli, ambapo leo tutaangali baadhi ya mambo yanayoweza kutusaidia kupata furaha ya kweli katika maisha yetu ya kila siku. Mambo hayo tutayatafakari kwa kujiuliza aina hii ya maswali.
A-Je tunapokuwa tunatafuta furaha tunatumia uwezo wetu wote au kwa kiwango kidogo? Kama tunatumia kiwango kidogo basi tujue kuwa hata kama tutapata kitu tunachodhani kitatufurahisha utajikuta hatufurahi, kwa sababu tulichopata kimeshindwa kukidhi matakwa yetu. Ili uwe na furaha ya kudumu tumia uwezo wako wote kutafuta kazi nzuri, biashra nzuri, mke mzuri ili uweze kufurahi kwa muda mrefu, la sivyo ulichopata kitakukinai mapema.
B- Je tunafanya sawa katika maamuzi au tunabahatisha tu? Endapo tutakuwa tunafanya mambo ya kubahatisha ambayo hatujayahakiki, huzuni yetu itakuwa kwenye makosa na kamwe hatuwezi kufanikiwa kupata yale tunayotaraji yatufurahishe.
Kuna watu wanatafuta watoto lakini hawazingatii kalenda za mimba na wengine wanatafuta mali, elimu kubwa, mke mwema, lakini hawako makini katika kufanya maamuzi kwa usahihi. Ni vema tukathibitisha uchaguzi wa mambo ili tufanikiwe kupata yatakayotufurahisha.
C- Je tunatimiza wajibu wetu au tunadanganya? Wapo watu ambao walitamani kuoa ili wapate furaha, lakini walipofanikiwa katika hilo hawakutimiza majukumu yao wakajikua wanageukwa na wake/waume zao na kujutia uamuzi wao. Msomaji wangu, unapokuwa katika safari ya kutafuta furaha kupitia utajiri, elimu, uongozi ni vema ukatimiza wajibu wako, ili upate matokeo mazuri.
Maana kama utakuwa unatamani kufaulu mtihani wako halafu husomi kwa bidii, sina shaka majibu utakayopata yatakuhuzunisha kwa sababu lazima ufeli na furaha uliyotaka haitapatikana. Chochote unachopata kitumikie kwa uwezo wako ili uone faida yake, maana kuna faida gani ya kununua gari au kujenga nyumba halafu usiitumie?
D- Je tunafuata muongozo, au tunakiuka? Kila jambo tunalotaka kulifanya lina kanuni zake. Kuendesha gari, kuwasha jiko la mafuta na kila kitu kina muongozo ambao mtu asipoufuata hawezi kuona matokeo sahihi. Namna yoyote ya kukiuka kanuni za utendaji lazima matokeo yatakuwa mabaya yatakayoweza kukuondolea furaha yako haraka.
E- Tunatumia tulivyopata au tunavitelekeza? Wapo watu ambao hutamani kupata kazi, lakini wanapopata hawazitumii, kazi hizo kwa ukamilifu, badala yake wanakuwa watu wa kufanya ujanja ujanja kwa kutoroka na wakati mwingine kutojihusisha na shughuli nyingine kwa lengo lile lile la kutafuta furaha.
Kusema kweli mtu wa namna hii hawezi kuwa na furaha kwa sababu anayolenga yamfurahishe hayatumii kufurahika na badala yake anatafuta jambo jingine. Fikiria kuhusu mume/mke anaoa lakini anaacha kumtumie mke/mume wake anakwenda kwa hawara! Sasa ni lini mtu huyo ataiona furaha ya kuwa mke au mume.
Soma vifungu hivi ndani ya kitabu cha Biblia “Vitu vyote ni halila, bali si vitu vyote ifaavyo.” (1 Wakorintho 10:23). “Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi” (Yakobo 4:17)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment