Sunday, November 25, 2012
Rasilimali Watu
Rasilimali watu ndiyo ya maana kuliko zote kwa sababu ina uwezo wa kugeuza rasilimali nyingine yote ili kuboresha maisha watu. Kuiendeleza na kuitumia barabara kunaongeza tija na thamani ya mtaji. Kwa hiyo maendeleo ya rasilimali watu lazima yawe ni lengo kuu katika ajenda ya maendeleo ya Taifa.
Serikali, wakati wote inatambua umuhimu wa juhudi za pamoja katika kuleta maendeleo ya rasilimali watu. Azimio la Arusha ndilo lililokuwa msingi wa malengo ya Taifa na mikakati, na hii ilijitokeza katika mfulilizo wa mipango ya maendeleo, na ambayo ilikuwa na malengo matatu: kukua kwa uchumi, usawa na kujitegemea, ikitilia mkazo maendeleo vijijini, watu wote kujua kusoma na kuadika, na upatikanaji wa mahitaji ya msingi kwa watu wote. Uboreshaji wa hali ya maisha ndiyo iliyokuwa msingi wa hatua na programu zilizotekelezwa kipindi cha baada ya uhuru. Yanayofahamika zaidi ni:
¨ Uhamasishaji wa watu wa Vijijini kujiunga na Vijiji vya Ujamaa, nia ikiwa kuhakikisha kuwa huduma za afya, elimu ya msingi na sekondari, elimu ya ufundi, pamoja na maji salama yanawafikia watu wote.
¨ Elimu ya msingi kwa wote ilifikiwa kwa zaidi ya asilimia 75 ya watoto wa umri wa kwenda shule kuweza kujiandikisha miaka ya 1970.
¨ Mipango ya elimu ya umma, ambayo ilifikia zaidi ya asilimia 80 watu wote wazima kujua kusoma na kuandika, na ukuzaji wa kiswahili kama lugha ya Taifa.
¨ Kuchanganya elimu na kazi (i.e. Azimio la Musoma) ikiwa ni na upanuzi wa shule za msingi, sekondari, ufundi na taasisi za elimu ya juu.
Mafanikio yaliyotajwa yalipatiakana kwa gharama kubwa kwa Serikali. Mkabala uliotumiwa ulikuwa wa Serikali kuingilia na kudhibiti, na hivyo kuendeleza urasimu pamoja na udhaifu wake, kama rushwa na uzembe. Zaidi ya hayo, mkabala uliotumiwa na Serikali uliwafanya wananchi wawe watazamaji wa maendeleo yao. Kwa hiyo kadri muda ulivyopita mipango yote ya kukuza rasilimali watu ya wakati huo ikawa si endelevu.
Wakati huu, Serikali imechukua mkabala mwingine unaoendana na hali halisi ya kijamii na kiuchumi katika Tanzania na dunia ya leo. Serikali inatambua mahitaji na dai la uchumi wa soko huria linalokabili taifa, mojawapo ni kwa wananchi wake kushindana katika soko huria la ajira kwa kutumia ujuzi na maarifa. Mkabala huu ni kwa misingi ya malengo ya sera mpya, ambayo ni kuonyesha umuhimu wa sekta binafsi, kuweka mkazo zaidi wa mahitaji ya wafanyakazi katika sekta ngazi ya usimamizi, na hatimaye kuachia nguvu za soko kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuunganisha mahitaji ya jamii na mipango ya kuendeleza nguvu kazi.
Mkabala wa kupanga rasilimali watu unafanyika katika ngazi tatu: kitaifa, kisekta na kiusimamizi. Pili, utambuzi huu kwa upande wa serikali una maana kuwa kuna haja ya kuwa na sera itakayohakikisha kuwa elimu na elimu ya ufundi katika ngazi za msingi na sekondari inahusika na mahitaji ya msingi ya soko la nguvu kazi, kwa kuwa na maarifa na stadi iliyopatikana kupitia elimu na mafunzo.
Tatu, kwa kuwa mkakati wa taifa wa maendeleo unashirikisha jamii nzima hadi vijijini, serikali inapanua elimu ya msingi kuhakikisha kuwa watoto wenye umri wa kwenda shule wanapata elimu hiyo; na kwamba wanafundishwa na kupata stadi za kiufundi zitakazowawezesha kujiajiri.
Njia nyingine mpya ya mpango wa serikali kuendeleza rasilimali watu ni kushirikiana na taasisi za binafsi na tasasi zisizo za kiserikali, pamoja na zile za jamii ili kutumia uzoefu walio nao wa kuwasiliana na wananchi katika ngazi za chini kabisa.
Nguvu-Kazi
Nguvu kazi katika Tanzania inakua kwa asilimia 3 kwa mwaka. Mwaka 1999 ilikisiwa kuwa 16,006,178. Zaidi ya nusu wako kwenye kundi la umri wa miaka 10-19, na asilimia kama 80 hivi wanaishi Vijijini. Karibu asilimia 8.5 ya nguvukazi ina zaidi ya elimu ya msingi au mafunzo. Wanawake ni chini ya nusu ya nguvukazi. Nguvukazi iliyo na elimu ni ndogo na iko zaidi mijini. Kwa jumla inakadiriwa nguvukazi mpya 500,000-600,000 huingia kwenye soko ka kazi kila mwaka, wengi wakiwa vijana.
Wastani wa asilimia 82 ya wafanyakazi wenye umri wa kuajiriwa wanajishughulisha na kilimo. Wengi wana kilimo cha kujikimu au hushiriki kwenye kilimo cha familia. Ijapokuwa walioajiriwa katika kilimo ni wachache, ajira za mara moja moja ni kitu cha kawaida.
Sekta isiyo rasmi(ukiondoa kilimo sehemu za vijjini) imekuwa kwa kasi kutokana na marekebisho ya uchumi na inachukuliwa kuwa ni chanzo endelevu cha ajira, ikiwa na asilimia 12 ya nguvukazi yote iliyoajiriwa. Kwa wastani aliye katika sekta isiyo rasmi pato lake kwa mwezi lilingana na yale ya sekta rasmi, hata kuzidi kima cha chini cha mshahara wa Serikali unaolipwa kwa wale wasiokuwa na ujuzi na utaalamu.
Sekta rasmi ina watumishi wa Serikali, mashirika ya umma, na makampuni binafsi ambao kwa pamoja ni kama asilimia 6 ya nguvukazi yote iliyoajiriwa. Sekta binafsi inaendelea kuwa muhimu kutokana na juhudi za kulegeza masharti na uchumi huria, na idadi watu walioajiriwa katika sekta rasmi ya binafsi imeongezeka mara dufu toka mwishoni mwa miaka ya 90.
Kuna matatizo tofauti yanayokabili miji na maeneo ya vijijini. Mijini, kutokuwa na kazi kabisa kuko juu, hasa kwa vijana. Kuna mfulilizo wa uhamiaji mijini kutoka vijijini, ikionesha sio tu kuweko kwa mishahara mizuri mijini, bali pia kutokuweko kwa nafasi za ajira vijijini.
Matarajio ya kukua kwa ajira yanapishana kati ya sekta na sekta. Kwa Sekta rasmi ya umma, ajira inatarajiwa kusimama. Ajira kwenye sekta rasmi binafsi inatarajiwa kuongezeka kwa kasi hasa kama mazingira ya kuwekeza yataendelea kuwa mazuri. Ajira katika sekta hiyo imekuwa ikikua kwa asilimia 9-10. Kama idadi watu vijijini na uchumi vitakua tunatarajia kukua kwa ajira kwenye viwango vya asilimia 2.5 na 3.0. Sekta isiyo rasmi inatarajiwa kutoa ajira mpya kama 100,000 kwa mwaka.
Pato la idadi kubwa ya Watanzania litaendelea kupatikana kutoka katika sekta ya kilimo. Ijapokuwa ajira katika kilimo itaongezeka sambamba na kasi ya ongezeko la idadi y6a watu vijijini, ubora na wingi wa nafasi hizi utategemea kiwango cha maendeleo ya Sekta ya Vijijini kwa jumla. Ili kuongeza ajira katika kilimo ni muhimu kuwa na mkakati wa maendeleo utakao- boresha miundombinu, elimu vijijini, ugavi wa bidhaa, umiliki wa ardhi, pembejeo na masoko, na kuweko bidhaa zitakiwazo. Juhudi hizi zitawezesha shughuli nyingine zaidi kuliko kilimo cha kujikimu, na hivyo kuongeza kipato kutoka kilimo, kwa kuwa na kazi nje ya kilimo itakaongeza mapato. Kuongezeka kwa nafasi za ajira katika kilimo vijijini ni muhimu sana ili kupunguza wingi wa ukosefu wa ajira mijini.
Sekta isiyo rasmi ina nafasi ya kutoa nafasi zaidi za ajira kwa ufanisi zaidi kuliko mashirika makubwa. Hata hivyo ajira nyingi katika sekta hii haziaminiki, na kuna uwezekano zisiongezeke. Hatua muhimu za kuongeza nafasi ya ajira katika sekta ni pamoja na kuendeleza mikopo ya zana, ambayo inaendana na hali za wakopaji wasiokuwa na dhamana; kuboresha upatikanaji wa mali ghafi na masoko, kutoa mafunzo ya ujuzi na kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi.
Upeo wa ajira katika sekta rasmi ya umma ni mdogo. Ukilinganisha, marekebisho ya uchumi yamekuwa na athari wazi za kukua kwa sekta rasmi ya binafsi. Marekebisho haya yanahitajika kuendelezwa ili kuongeza ukuaji kwa kasi zaidi.
Uboreshaji wa elimu ya misingi na sekondari ni muhimu sana katika kuongeza matarajio ya ajira. Aina mbali mbali za mafunzo yanahitajika ili kupunguza ukosefu wa stadi. Hii inawezekana kwa kurekebisha mitaala iliyopo na kuhakikisha inaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.
Sera
Kwa sasa, hakuna sera moja inayotawala maendeleo ya rasilimali watu kwa sekta zote. Hata hivyo zipo sera hapa na pale katika sekta mbali mbali zinazohusu maendeleo ya rasilimali watu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment