Sunday, November 25, 2012
UFANYEJE KATIKA HALI NGUMU YA UCHUMI?
Matatizo ya ugumu wa uchumi katika dunia hii siyo mapya. Tangu baada ya mwanadamu kuanguka katika dhambi – amekuwa mara kwa mara akisumbuliwa na matatizo ya uchumi. Ukisoma habari za Isaka na za Yakobo utaona jinsi hali hii ilivyojitokeza.
Lakini biblia inaeleza wazi kuwa siku hizi ni mwisho. Katika siku hizi za mwisho, biblia pia inasema wazi kabisa kuwa dunia itapita kwenye vipindi vigumu vya uchumi
Kwa Mfano: Katika Mathayo 24:7 na Ufunuo wa Yohana 6:3-6 tunaona ya kuwa katika siku hizi za mwisho kutatokea njaa – au upungufu wa chakula. Sababu ya kuja kwa njaa hiyo ni vita vitakavyokuwa vinatokea katika nchi mbalimbali. Ni wazi kabisa kuwa palipo na vita au palipo na ugomvi, panakuwa na matatizo ya ulimaji mashamba na usafiri wa kuleta chakula toka sehemu zingine. Matokeo ni hilo eneo au nchi kukosa chakula, haya mambo yaliyotabiriwa kutokea siku hizi za mwisho wa dunia.
Ukisoma katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana sura za 17 na 18 utaona ya kuwa hali ngumu ya kibiashara imetabiriwa kutokea katika siku hizi za mwisho. Kuuza au kununua kutafanyika kwa vibali. Watu watapenda fedha sana kuliko kumpenda Mungu. Kutakuwa na uhusiano mkubwa sana kati ya utajiri na biashara na uasherati. Wafanya biashara wa siku hizi za mwisho watakuwa na sehemu kubwa katika utawala wa miji au vijiji wanavyokaa – hata wakati mwingine katika maongozi ya nchi au mataifa mbalimbali.
Matokeo ya hali namna hii inawafanya watu watafute njia au mbinu za kuweza kuishi katika vipindi vya namna hiyo. Lakini ni wazi kuwa si mbinu zote au njia zote ambazo wanadamu wanazitumia katika kuishi wakati wa hali ngumu ya uchumi zinampendeza Mungu.
Kunapotokea hali ngumu ya uchumi, tabia za watu zinabadilika. Mara kwa mara mambo yafuatayo hutokea;
Kubana matumizi Kununua vitu kwa wingi na kuvirundika Uchoyo – kupunguza tabia ya utoaji na ukarimu Watu huacha kumtumikia Mungu na badala yake mtu huitumikia mali Rushwa, wizi na dhuluma huwa ni vitu vya kawaida Miradi ya kila namna huibuka kuanzia kwa watoto hadi watu wazima.
Jambo linalowafanya watu wawe na tabia hizi, ni lile la kutaka kutafuta namna ya kuishi katika kipindi kigumu cha uchumi. Je!mkristo afanye nini ili aishi katika kipindi hiki kigumu cha uchumi bila kufanya mambo yatakayomkosea Mungu?
Wakristo wengine wamefika mahali pa kuhalalisha miradi ya kuwapatia fedha ambayo ni kinyume na ushuhuda wa kikristo – Je! hii ni sawa?
Wengine wamefika hata mahali pa kufunga nira na wasioamini (wasio wakristo) KWA JINSI ISIYO SAWASAWA (yaani isiyokubalika) na neno la Mungu ili waweze kupata fedha kutokana na mradi wanaofanya pamoja. IKO "jinsi iliyo sawasawa" na utaifahamu ikiwa utakuwa mtendaji wa neno la Mungu.
Wakristo si wa ulimwengu huu
Ndugu au Dada unayesoma sasa mambo haya – sikiliza! Sisi kama wakristo si wa ulimwengu huu ingawa tunaishi hapa ulimwenguni. Fahamu na kumbuka hili kila wakati. Yesu Kristo alisema hivi;
"Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni" (Yohana 17:14-18).
Je! unafikiri Yesu Kristo anaweza kututuma hapa duniani bila kutuandaa kuishi kiushindi katika majaribu yaliyomo ndani yake na hali ngumu ya uchumi?
Je! unadhani Yesu Kristo anaweza kukuokoa halafu asikutunze kiuchumi katika maisha mapya ya wokovu? Nafahamu kuna wakristo wengi walioanguka kiroho kwa sababu ya kutafuta njia za kujisaidia kimaisha.
Biblia inatuambia ya kuwa Yesu Kristo huwalisha na kuwatunza watu wake ili ajiletee kanisa (wakristo) walio watakatifu. Soma Waefeso 5:25-33.
Katika vipindi vyote vya matatizo ya uchumi, Mungu ameweza kuwalisha na kuwatunza watu wake. Wamekula na kuvaa na kulala ndani ya mpango wake bila kumkosea.
Katika siku hizi za mwisho, Kristo anazungumza na kulikumbusha kanisa (wakristo) juu ya njia au mbinu za kuchukua wakati wa hali ngumu ya uchumi mahali walipo.
Mashauri muhimu ya kufanya
Fuata maongozi ya Mungu na siyo ya dunia: Ni rahisi sana kusikia na kufuata ushauri wa wanadamu kuliko ushauri wa Mungu hasa mtu anapobanwa na shida. Lakini kwa mkristo nakushauri siku zote kuwe na shida au kusiwe na shida, fuata ushauri wa Mungu kama vile anavyokuongoza kwa Roho Mtakatifu katika neno lake. Tuangalie jinsi Isaka alivyofanya alipokumbwa na hali ya njaa.
"Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Ibrahimu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari. Bwana akamtokea, akasema, usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia …. Nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki …" (Mwanzo 25:1-3).
Njaa ilipotokea huko Gerari, watu walianza kuondoka huko na kwenda Misri, ili kutafuta chakula. Ni wazi ya kuwa hata Isaka alitaka kufanya hivyo. Bwana akamzuia akamwambia asiondoke bali akae katika nchi aliyomwambia na katika nchi hiyo atakuwa pamoja naye na kumbariki au kumfanikisha.
Nataka kukukumbusha ya kuwa baraka za Mungu kwetu hazitegemei jinsi hali ya hewa na uchumi wa dunia hii unavyokwenda bali zinategemea NENO LA KRISTO.
Isaka akatii, hakuondoka bali alibaki katika nchi hiyo ambayo watu walikuwa hawapati chakula wakilima.
"Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, Bwana akambariki" (Mwanzo 26:12).
Siku zote kaa na kufanya kazi mahali ambapo Mungu amekuongoza kukaa. Usihame mahali au kuacha kazi, bila uongozi wa Mungu. Kufanikiwa kwako hakutegemei mipango yako bali kunategemea mpango wa Mungu.
Ukiwa ndani ya Kristo utafanikiwa mahali po pote pale ambapo Mungu atakapokuweka hata kama mazingira yake kibinadamu si mazuri kwa kufanikiwa. Ukiwa ndani ya Kristo, "Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani … utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa utokapo …. Bwana ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako" (Kumbukumbu ya Torati 28:3,6,8).
Endelea kutoa hata wakati wa upungufu
Katika hali ya kibinadamu upungufu unapotokea mahali watu wanabana matumizi – na hali ya ukarimu na utoaji huwa inafifia sana hata wakati mwingine kupokea kabisa. Wakristo wengi pia wamekumbwa na hali hii – wanasema wamepunguza utoaji kwa kuwa wamepungukiwa na hali ya uchumi ni ngumu. Je! hii ni sawa?
Wakati wa ukame ulipotokea wakati wa maisha ya Nabii Eliya Mtishbi; Bwana alimwambia Eliya, "Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe" (1Wafalme 17:9).
Unakumbuka jinsi yule mama alivyojitetea wakati Eliya alipofika kwake ili alishwe? Yule mama alijitetea kama watu wengine wanavyojitetea siku hizi wakitakiwa kutoa au kuchanga walivyo navyo kwa ajili ya kazi ya Mungu. Naye yule Mjane akasema;
"Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tule tukafe" (1Wafalme 17:12).
Kwa jinsi ya kibinadamu, Eliya angeweza kumwonea huruma yule mama, asile chakula chake; na aondoke na aende kwa matajiri wa siku zile kupata chakula. Lakini Eliya hakufanya hivyo- bali ALITII MAAGIZO YA MUNGU. Eliya akamwambia yule mjane hivi;
"Usiogope;enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie KWANZA mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao" (1Wafalme 17:13).
Ndivyo yule mama alivyofanya – alimpa KWANZA MUNGU kwa kupitia mtumishi wake. Mungu akambariki yule mama kwa ukarimu na utoaji wake wakati alipokuwa na upungufu. "Lile pipa la unga HALIKUPUNGUKA, wala ile chupa ya mafuta HAIKUISHA sawasawa na NENO LA BWANA alilolinena kwa kinywa cha Eliya" (1Wafalme 17:16).
Katika hali ya upungufu ulionao, usiwe mchoyo bali endelea kumtolea Mungu, naye atakubariki na kukufanikisha. Na hii itaonyesha ni kwa kiasi gani unamtegemea Mungu wako na Neno lake.
Lazima ufahamu ya kuwa Yesu Kristo anaangalia sana jinsi tutoavyo. Siku moja akiangalia jinsi watu watoavyo fedha; "Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la Hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia" (Marko 12:43-44). Soma na kuyatafakari tena maneno hayo ya Yesu Kristo, halafu jiangalie jinsi utoavyo. Huyu mjane hakuwa na mali ya kutosha alikuwa maskini, lakini bado aliendelea kumtolea Mungu! Je wewe una la kujitetea katika kutomtolea Mungu wakati wa upungufu wako?
Weka hazina yako mbinguni
Yesu Kristo alisema;"Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo,na wezi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wezi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako" (Mathayo 6:19 – 21).
Utoaji wako utaonyesha kama moyo wako uko kwa Yesu au unaitegemea dunia. Moyo wako ukimtegemea sana Yesu, utatoa zaidi kwa ajili ya kazi ya Mungu kuliko mahali pengine. Mkristo anapopoa kiroho, utoaji wake HASA kwa kazi ya kuhubiri injili nao unapungua. Hata hivyo Biblia inatuambia katika siku za mwisho upendo wa wengi utapoa.
Mtolee Mungu zaka na dhabihu (matoleo) bila kuchoka, nawe utakuwa umeweka hazina yako mbinguni – mikononi mwa Mungu – ambamo wezi hawawezi kukuibia. Naye Bwana atakurudishia mara nyingi zaidi. Mradi mzuri na wenye uhakika wa mavuno kwa Mungu na kwako wakati wa hali ngumu ya uchumi ni mradi wa kuhubiri injili. Kwa hiyo siku zote hakikisha umeweka kiasi fulani katika mradi wa kuhubiri injili.
Dumu katika maombi
Hili ni muhimu sana. Kwa kuwa wakristo wengi wakiwa katika hali ya ugumu wa maisha na uchumi, wanapoa katika maombi – na wanakumbwa na majaribu ambayo mara nyingi yanachafua ushuhuda wao. Soma Luka 21:36, Mathayo 24:42 – 51 na Mathayo 26:41. Kwa hiyo dumu katika maombi, usikate tamaa, hata wakati wa hali ngumu kiuchumi kwa upande wako – bado zidi kudumu katika maombi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment