Sunday, November 25, 2012

JIFUNZE KUJITHAMINI ILI UTHAMINIWE

Msimamo wako au vile unavyoviamini vyaweza kuonekana tu katika vile ulivyo tayari kuvisimamia au kuvitetea. Kwa mfano, kwa sababu ya misimamo fulani binafsi mtu anaweza kuwa tayari kuwapoteza marafiki zake ili tu kuusimamia msimamo wake au kukisimamia kile anachokiamini. Tuchukue mfano wa kijana anayeamini katika uaminifu akiwa ofisini, mara unatokea upenyo wa kupata fedha fulani ya magendo ikiwa yeye ataidhinisha tu matumizi ya fedha hiyo, marafiki wote wanamsisitiza na kumshawishi kufanya hivyo ili watajirike, kwa sababu ya kile anachokithamini kijana huyu aweza kuwa tayari kuwapoteza marafiki zake wote ili tu kukilinda kile anacho kisimamia. Misimamo hii au Maadili haya binafsi huzaliwa wapi? Mara nyingi misimamo binafsi na maadili binafsi hujengewa misingi yake nyumbani, jinsi familia uliyokulia inavyoamini, jinsi baba au mama au ndugu uliokuwa nao muda mwingi wanavyo amini inaweza kuathiri kuamini kwako. Waweza kujiuliza ni nini familia uliyotokea au uliyoko inachokiamini, nini inacho kihisi, nini inachokiwaza, nini inachokitilia mkazo na nini inachokipa kipaumbele? Maadili na misimamo binafsi yote iliyochimbukia majumbani kwetu kukaa na kudumu sana ndani yetu. Sehemu ya pili ambapo maadili na misimamo binafsi hii huundwa ni kutoka kwa waalimu wa dini, waalimu mashuleni, marafiki, vyombo vya habari n.k Misimamo yote hii tunayoipata kutoka kote huku niliko kutaja yaweza kuwa mibaya au mizuri, yaweza kuwa ya msaada au ya kuhatarisha. Katika hili basi tunapata aina mbili kubwa za maadili ambayo yanaweza kuiongeza thamani yako au kuipunguza sana thamani hiyo. Maadili mabaya (Negative values): Hivi ni vile vitu, au mambo ambayo kwa kuyafanya yanaweza kukudhuru, kukuharibu, kukuumiza au kukuhatarisha wewe na wengine pia. Mfano; Ubinafsi, uchoyo, magomvi, wizi na udokozi, kutokutii, uchafu n.k Maadili mazuri (Positive values): Hivi ni vile vitu au tabia ambazo hazimhatarishi wala kumdhuru mtu wala wale wanao mzunguka badala yake zinamjenga na kumuongezea uthamani wake na hivyo kumfanya azidi kuwa mtu wa watu.Mfano; Kuwa mkweli, mwaminifu,, upendo, hekima, utii, usafi, juhudi, bidii n.k Mtu yeyote asiyejithamini utu na hadhi yake nirahisi sana kujikuta anaangukia katika maadili na tabia mbovu kwa kujijua au hata bila kujitambua, wakati yule mwenye kujithamini yeye mwenyewe mara kwa mara hufanya yale yaliyo bora kwake na kwa wengine pia. Hata kama mazingira uliyozaliwa au kukulia hayakuruhusu wewe kuthaminiwa na waliokuwa wanakuzunguka na hiyo ikapelekea wewe kutojithamini mwenyewe, leo tupilia mbali mtazamo huo hasi. Amini kwamba kutothaminiwa na wengine hakuwezi kuwa ufunguo wa mimi kutokujithamini mwenyewe, hatakama ulimwengu na walimwengu hawajaitambua thamani yangu mimi ni wakwanza kuijua na hivyo ni lazima niithamini. Ingawa tuko wengi na wengine yamkini wanafanana na mimi lakini ukweli unabaki palepale kuwa mimi ni wa thamani kwasababu hakuna wa aina yangu mwingine kokote. Jifunze kusema leo “I AM SPECIAL”.

No comments:

Post a Comment