Sunday, November 25, 2012

JENGA USTAWI KATIKA BIASHARA

KONA YA WAJASIRIAMALI: KARIBU msomaji wa kona ya wajasiriamali, hii ni kona ambayo maudhui yake ni kuona namna bora ambazo wajasiriamali wanaweza kuzitumia ili kuanzisha na baadae kuendeleza biashara zao na kupata mafanikio wanayotamani. Nawashukuru wasomaji wa kona ya wajasiriamali ambao wamekuwa wakinipa mrejesho kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu, wengi wamekuwa na maswali mbalimbali juu ya ujasiriamali pamoja na kutaka kufahamu juu ya kupata mikopo nafuu na taratibu zake. Katika kona ya wajasiriamali leo, tutaona juu ya namna bora ya kujenga ustawi katika biashara. Lengo la kujenga ustawi katika biashara yako ni kupanga na kujenga maendeleo endelevu, kuwa na namna ya kufanya biashara idumu. Ndugu mjasiriamali, katika biashara unayofanya iwe aidha mpya au iliyokomaa, ni muhimu kujiwekea utaratibu wa kupitia madhumuni hasa ya kile unachofanya, na hili linaweza kufanyika kila baada ya kipindi fulani kwa mfano mwaka mmoja. Lengo kuu la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa unalenga shughuli moja au chache ulizoamua kuzifanya na kuzisimamia vizuri na kwa ufanisi. Hii itakurahisishia kuweka madhumuni na malengo unayoweza kuyatimiza na kupata matokeo tarajiwa. Mjasiriamali, kumbuka juu ya namna bora ya kupunguza hasara ya rasilimali unazotumia katika biashara, ikiwemo matumizi ya fedha za biashara, na kila wakati jiwekee utaratibu wa kutofautisha matumizi ya fedha za biashara kwa mambo binafsi na biashara. Ni wazi kuwa mjasiriamali mpya au mwenye uzoefu na mambo ya biashara, wote wana kiu ya kuongeza kipato na rasilimali mbalimbali katika biashara zao. Kiu hii ya wajasiriamali itafikiwa tu kwa kujenga utamaduni wa kufikiria kesho. Wajasiriamali wanaposhauriwa kufikiria kesho wanatakiwa kuelewa kuwa, kujenga ustawi katika biashara si suala la kulala na kuamka, unahitaji kujenga nidhamu katika biashara, kumbuka msemo usione mbuyu umekua nao ulianza kama mchicha! Ili kujenga mazingira mazuri ya kufikiria kesho, yafaa kwa wajasiriamali kujiuliza maswali mbalimbali ambayo yatakuwa na majibu yatakayotoa mwelekeo wenye kufaa ambao utaisaidia biashara kupata ustawi, baadhi ya maswali ya kujiuliza ni kama vile: Mosi, kwanini unafanya biashara hii unayoifanya? Swali hili litakupa wasaa wa kujitathmini na kupima mwelekeo wa kile unachokifanya. Kwa swali hili utapata mchanganuo wa sababu za wewe kufanya bishara husika. Vile vile swali hili litakupa majibu ya kwanini uliamua kutumia nguvu na mali zako kufanya biashara hiyo na si nyinginezo. Yafaa kukumbuka wapo wajasiriamali ambao walishindwa biashara kutokana tu na kufanya yale ambayo wengine wanafanya. Wengi kwa macho waliona wenzao wamefanikiwa katika biashara fulani, kwa mfano biashara ya mazao, na kuamua nao kujiingiza katika biashara hiyo bila kufanya tathmini kama wataweza kuhimili changamoto zilizomo katika biashara hiyo. Swali la pili, ni, je katika kipindi cha muda fulani kwa mfano miaka mitatu ungependa biashara yako iwe katika hali gani? Usifanye mambo kimazoea, jiwekee malengo yatakayokuwa chachu ya wewe kupata mafanikio katika biashara yako. Hili ni swali ambalo linamjenga mjasiriamli kufikiria kesho, na ili kujenga kesho yenye kuleta ustawi yafaa kujiwekea vigezo mbalimbali katika biashara ili kwa kuvisimamia vema uweze kuandaa mazingira ambayo yatakusaidia kufikia mafanikio katika biashara. Swali la tatu la kujiuliza, je unahitaji kitu gani ili uweze kufikia malengo yako? Lengo la swali hili ni kujua yale yaliyo muhimu ili uweze kujenga ustawi katika biashara unayofanya, je unahitaji vitu gani zaidi ili uweze kupata mafanikio ya kweli ? Kaa chini ufikirie yale ambayo unayahitaji ili kupata mafanikio ya uhakika. Kwa mfano yafaa kujiuliza je bidhaa au huduma unayotoa ina ubora gani, je wateja wa biashara yako ni kina nani hasa, ni kwa njia gani unaweza kuongeza idadi ya wateja wako. Je bei zako zinaendana vipi na hali ya soko, je bidhaa au huduma yako inawafikiaje wateja, je wateja wako wanaridhishwaje na huduma unayotoa kwao. Maswali haya na maswali mengine yakusaidie kupata namna bora ya kujenga ustawi wa biashara. Swali la nne la kujiuliza, ni vikwazo gani unahitaji kuvivuka ili uweze kufikia malengo tarajiwa ? Ndugu mjasiriamali yafaa kukumbuka kila wakati vikwazo mbalimbali ambavyo vinaweza kuwa sababu ya wewe kurudi nyuma kibiashara. Baadhi ya vikwazo vya kujiuliza ili kujenga ustawi katika biashara yako na hatimaye kufikia malengo yako ni pamoja kutathmini udhaifu ulio nao katika kuendesha biashara yako. Kumbuka huwezi kuwa mzuri kwa kila jambo, utakuwa na mazuri na mabaya. Jipime wewe na washindani wako kwa mfano, je kiwango cha huduma bora kwa wateja kikoje ukifananisha na washindani wako ? Wapo wajasiriamali ambao wana kila kitu ambacho wateja wanahitaji lakini wanashindwa kutoa huduma bora kwa wateja wao. Pamoja na maswali haya ambayo yanaweza kutoa mwelekeo wenye kufaa wa namna bora ya kujenga ustawi katika biashra yako, yafaa pia kukumbuka baadhi ya vitu ambayo vitasaidia kujenga ustawi na kukupa mwelekeo wa mafanikio katika biashara yako. Inashauriwa kuwa na shughuli chache unazozimudu vema. Kuwa na shughuli ambazo utazimudu kwa kuzisimamia vema, wapo wajasiriamali ambao wameshindwa kufanikiwa kutokana na kuwa na shughuli nyingi na kushindwa kuzisimamia vema. Ili kujenga ustawi katika biashara yafaa madhumuni ya biashara yako yafahamike na kueleweka vema. Kwa mfano kama una wafanyakazi yafaa waelewe kwa nini kinafanyika hicho kinachofanyika, hii itawasaidia nao kutimiza wajibu wao vema. Ndugu mjasiriamali, ili kujenga mwelekeo wa mafanikio katika biashara yako, yafaa kuwa na mchanganuo mzuri wa wateja wako. Yafaa kuzingatia mahitaji ya soko na andaa rasiliamali zenye kufaa ili kutoa huduma bora kwa wateja. Jenga utamaduni wa biashara yako kuwa bora, wewe kama mjasiriamali na mmiliki wa biashara husika yafaa uwe mfano wa kuigwa na wengine katika biashara yako, kuwa mtu wa mfano. Jijengee mazingira ya kudumisha ubora wa biashara na bidhaa kila wakati. Kwa mfano, usimwajiri ndugu yako katika biashara kwa kuwa tu hana kazi, bali aajiriwe kwa kuelewa sababu ya biashara kufanyika na vigezo vyenye kufaa ili aweze kuwa sehemu ya biashara kuendelea vema na kupata ustawi na si kuwa tatizo. Tafuta namna bora ya kuwathamini wafanyakazi wako ili waweze kuelewa malengo yako vema. Jenga utaratibu wa kutambua mchango wa wafanyakazi wako kwa kuwapa motisha, kutokutambua michango yao katika biashara yako kunaweza kukugharimu. Lingine la kuzingatia ni kujenga utamaduni wa kusimamia vema fedha za biashara yako. Hata kama umemuweka mfanyakazi, fanya tathmini ya fedha kwa kuzingatia mapato, matumizi na gharama za biashara ili biashara yako iweze kuwa endelevu. Jiwekee namna bora ya kutunza kumbukumbu za biashara yako. Epuka mazoea ya kutembea na kumbukumbu kichwani mwako. Haiwezekani kuyakumbuka matukio yote ya juma, mwezi au mwaka bila kufanya marejeo kwenye kumbukumbu. Ni matumaini yangu ndugu mjasiriamali, kama utazingatia vema haya ambayo tumejikumbusha leo juu ya namna bora ya kujenga ustawi wa biashara, utakuwa mwanzo mzuri wa wewe kujenga mwelekeo wa mafanikio katika biashara yako.

No comments:

Post a Comment