Sunday, November 25, 2012

NAMNA YA KUANZISHA BIASHARA.

Ukitaka kufanya biashara yoyote ile unatakiwa kufanya utafiti. Kutokufanya utafiti ni chanzo cha biashara nyingi kuharibika. Lazima ujiulize kwamba unataka kufanya biashara gani? Usiseme unataka kufanya biashara yoyote ile kwani kusema kwamba unataka kufanya biashara yoyote ile ni kupoteza mwelekeo kwa kuwa utakuwa hujui unataka kufanya nini. Kama hujui cha kufanya hakuna kitu utakachokifanya. Hili ni tatizo la watu wengi. Hata baadhi ya watu niliokutana nao wakitaka ushauri wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo hili. Njia ya kukusaidia kuamua ufanye biashara gani ni kwa kujiuliza umewahi kufanya kazi au biashara gani? Umesomea nini? Vipaji vyako ni vipi? Ni biashara ipi au kazi ipi unapenda zaidi kuliko nyingine na kwa sababu gani? Ukisha jiuliza maswali haya chukua kalamu na karatasi uandike maswali yako na kuyajibu. Ukikagua maswali na majibu yako utagundua shughuli unayoipenda, unayoiweza na una kipaji nayo na hiyo ndiyo inayokufaa. Ukishachagua biashara unayoipenda ni rahisi sana kufanikiwa kwani shughuli utazifanya kwa hiyari bila kujilazimisha. Kama unashindwa kuamua ni biashara gani ufanye, soma sura ya sita katika kitabu hiki. Nimeelezea kuhusu mawazo yanayoweza kukusaidia kuanzisha biashara mbalimbali ambazo unaweza kuzifanya. Kama utakuwa bado hujafikia uamuzi baada ya hapo basi tafuta na wasiliana na washauri ili mbadilishane mawazo na ufundishwe jinsi ya kuamua ufanye biashara gani. Mambo mengine unayotakiwa kuyafanyia utafiti ni:- (i) Kujua siri ya bishara unayotaka kufanya ili upate mbinu za kupata mafanikio. Unaweza kupata siri au kujifunza mbinu kutoka kwa watu wanaofanya biashara kama unayotaka kufanya. Suala hili ni gumu sana kwani wafanyabiashara wengi huwa wanaficha siri za biashara zao ili kulinda wasizidiwe maarifa na washindani wao. Unaweza kuipata siri hiyo kama utakwenda kupata ushauri toka kwa mfanyabiashara ambaye yuko mbali na mahali unapofanyia biashara, au tafuta ushauri kwa wataalamu wa mambo ya biashara. (ii) Fanya utafiti wa soko la bidhaa unazouza au unazotarajia kuuza. Jiulize, je bidhaa unazotaka kuziuza zina soko? Utawauzia watu gani na utauzaje? Kama wewe ni mzalishaji, una mazao / bidhaa unapaswa kuuza kwa jumla, mchanganyiko ama rejareja? Je utatangaza vipi bidhaa zako? Maelezo ya namna ya kutangaza bidhaa zako utayapata katika Sehemu ya Tatu ya Kitabu hiki. Utafiti wa soko unaweza kuufanya kwa kuwauliza wafanya biashara waliotangulia maswali hayo ya utafiti kwani wao wamekuwapo kwenye soko na wanazijua siri za soko. (iii) Tengeneza bajeti yako kwa kuorodhesha vitu vinavyohitajika na gharama zake ili kuweza kuanzisha biashara yako. Vitu hivyo ni:- (a) Gharama za Kujenga au kupanga ofisi (b) Gharama za Leseni ya biashara (c) Makadirio ya kodi toka TRA (d) Garama ya vifaa vya ofisi yaani, Samani, makaratasi, mitambo, mashine, nk (e) Manunuzi ya malighafi au bidhaa za kuanzia biashara (f) Idadi ya wafanyakazi na gharama za mishahara yao. (g) Gharama nyinginezo kama vile, umeme, maji, nk. (iv) Unatakiwa kujua ni mtaji kiasi gani unahitajika kuanzisha biashara yako. Mtaji huo utaujua baada ya kujumlisha gharama zilizoorodheshwa katika kupengele namba (iii)Gharama hizi ni za mwaka ule wa kwanza wa kuanzia (v) Tafuta Mtaji. Mtaji unaweza kupatikana kutoka kwenye vyanzo vifuatavyo:- (a) Akiba au mshahara (b) Msaada au mkopo kutoka kwa ndugu na jamaa. (c) Kuingia ubia na mtu mwenye mtaji (d) Mkopo toka baadhi ya asasi kama vyama vya akiba na mikopo (SACCOS), NGO za kifedha sipokuwa Benki kwani hizi huwa hazitoi mikopo kwa mtu anayeanzisha biashara. TARATIBU ZA KISHERIA ZA KUFUATA ILI KUANZISHA BIASHARA Baada ya kufanya utafiti na kupanga mipango ya kuanzisha biashara unatakiwa kwanza kuangalia taratibu za kisheria ambazo unatakiwa kuzifuata na kuzitekeleza. Kama biashara yako ni ndogo anza kama mtu binafsi. Faida ya kuanza biashara kama mtu binafsi ni urahisi wa kuanzisha biashara; urahisi na wepesi wa kutoa maamuzi kwani huhitaji ridhaa ya mtu mwingine kabla ya kutoa uamuzi; mtaji unaohitajika utakuwa mdogo kutokana na gharama za uendeshaji kuwa ndogo, biashara hii inaweza kuendeshwa kwa msaada wa familia kwa kumtumia mke au mume, watoto au ndugu na jamaa na raslimali za familia kama nyumba na samani. Unapoanzisha biashara na kuiendesha mwenyewe unakuwa huru tofauti na mifumo mingine. Matatizo ya kufanya biashara kama mtu binafsi ni:- Kushindwa kupanua biashara yako kwa ufinyu wa mtaji; kufilisiwa mali zako za binafsi iwapo biashara yako itafilisika kwani katika mfumo huu mali ya biashara na mali binafsi si rahisi kuzitenganisha; Kuongeza mtaji inakuwa ni vigumu, hivyo unaweza kushindwa kupanua biashara yako. Ili kuepukana na matatizo niliyoyataja hapo juu unaweza kuungana na watu wengine kufanya biashara kwa ubia. Faida za kufanya biashara kwa ubia ni: Kupata fursa ya kuongeza mtaji kwa kushirikiana na wafanyabiashara wengine ambao wataleta mitaji yao; Kuongeza ujuzi katika shughuli kwa kuleta wataalamu pale taaluma Fulani inapohitajika. Matatizo ya kuendesha biashara kwa njia ya ubia ni: Kufilisiwa mali zako binafsi endapo biashara yako itafilisika; kudhulumiana mali endapo moja wa wabia atakuwa si mwaminifu ambapo anaweza kuingia mikataba mibovu na kusababisha hasara ambayo itabebwa na wabia wote. Ni muhimu kuwachunguza watu tunaotaka kujiunga nao ili tujue kama ni waaminifu. Pia ni vyema kuwapo na mkataba wa maandishi mnapoanzisha biashara ya ubia mkimshirikisha mwanasheria kama shahidi ili kujikinga na kudhulumiana; Kufariki kwa mbia mmoja kunaweza kusababisha kuvunjika kwa ubia; kotokuelewana kwa wabia kunaweza kusababisha kuvunjika kwa ubia. Kama biashara ikikua unaweza kuanzisha kampuni. Mfumo wa uendeshaji wa kampuni unazo faida zifuatazo: unatenganisha majukumu ya wamiliki mali na kampuni yaani kampuni inaposajiliwa inakuwa inakuwa na hadhi na kutambulika kisheria kama ni mfumo tofauti na wamiliki. Mfumo huu unatenganisha majukumu kati ya menejimenti na wamiliki wa kampuni; madeni ya kampuni yatalipwa hadi kufikia kikomo cha mtaji uliowekezwa na wamiliki. Hivyo, mali binafsi za wamiliki wa kampuni haziwezi kukamatwa kufidia madeni ya kampuni endapo kampuni itafilisika. Mfumo wa kampuni unatoa nafasi ya kupanua mtaji kwa kukusanya mitaji kwa kuongeza wanahisa au kupitia soko la mitaji ya hisa. Mfumo huu ndiyo unafaa kwa biashara kubwa kwani unatoa nafasi ya kupanuka kwa biashara na kuendelea kuwapo kwa biashara hata kama baadhi ya wamiliki wake wakifa au kujitoa katika kampuni. Mambo ya muhimu ya kutekeleza kisheria kabla ya kuanzisha biashara ni:- (a) Kuwa na ofisi (b) Kukata leseni (c) Kusajiliwa na TRA kama mlipokodi na kupewa namba ya mlipakodi (d) Kufanyiwa makadirio ya kodi ya mapato ya awali (e) Kutimiza masharti mengine ya keshiria kuwa mfano kama wewe unataka kufanya biashara ya ukandarasi wa ujenzi wa majengo lazima usajiliwe kwenye Bodi ya Wakandarasi. Kama unafanya biashara ya kati au kubwa unapaswa kufuata sheria. Ni makosa kufanya biashara bila kufuata sheria za nchi. Hata hivyo, kuna biashara zingine ndogo ndogo sana kiasi kwamba uanzishaji wake si rahisi kufuata sheria hizo hapo juu, mfano uuzaji wa maandazi, karanga na vitu vingine vidogovidogo. Hizi zinaitwa biashara zisizo rasmi au biashara ndogondogo. Ni vyema ukachunguza kama biashara unayoifanya ni ndogo au kubwa ili ujue kama unapaswa kufuata taratibu za kisheria au la, kwani kutokujua utaratibu na sheria siyo kinga ya kukufanya usishitakiwe. CHARLES MSULUZYA NAZI Mwandishi wa makala hii ni mshauri wa biashara na mtunzi wa kitabu cha Mbinu za biashara na maarifa ya kupata pesa na utajiri. Kwa mawasiliano piga simu namba 0755394701 barua pepe cnazi2002@yahoo.com au tembelea tovuti yake www.mshauriwabiashara.com Mfahamu mwandishi wako wa makala za ujasiriamali Watu wengi wamekuwa wasomaji wa makala zangu kwa muda mrefu bila kunifahamu, na wengine wamekuwa wakinipongeza kwa kazi nzuri ya makala nilizoandika. Kwa leo ningependa niwaeleze mimi ni nani ili mnifahamu vizuri. Mimi naitwa Charles Paul Msuluzya Nazi ambaye ni mwandishi wa makala za ujasiriamali katika gazeti la Mtanzania kila siku ya jumanne. Nilizaliwa mwaka 1958 huko Mbogwe Wilaya ya Bukombe na nilisoma Shule ya Msingi Mbogwe na baadaye Sekondari Ihungo mwaka 1975 hadi 1978 ambapo baada ya kumaliza kidato cha nne nilijiunga na Chuo cha Ushirika na maendeleo ya jamii Tengeru. Baada ya kumaliza mafunzo niliajiriwa na serikali nikiwa ni Afisa Ushirika msaidizi wilaya ya Mahenge mwaka 1981 hadi 1983 ambapo nilijiunga na Shirika la Masoko Kariakoo nikiwa ni Mkaguzi wa mahesabu ya ndani. Mnamo Mwaka 1988 nilijiunga na Shirika la Umeme TANESCO nikiwa ni Mkaguzi Mwandamizi wa mahesabu ya ndani, ambako ndipo nilipo hadi sasa. Mbali na kufanya kazi za za Mwajiri wangu nimekuwa pia nikijishughulisha na kazi zangu binafsi pamoja na kuhudumia jamii. Miongoni mwa kazi nilizozifanya ni Kuongoza Soko kuu SACCOS nikishika nafasi ya Katibu na Mweka hazina kuanzia mwaka 1985 hadi 1988. Katibu wa TANESCO SACCOS toka 1997 hadi mwaka 2005. Pia mnamo mwaka 2005 na 2010 nilishiriki katika kura za maoni kuomba kugombea Ubunge wilaya ya Bukombe na jimbo la Mbogwe kupitia CCM ambapo sikupata kura za kutosha kuteuliwa kugombea ubunge. Mimi nimeoa na katika familia yetu tumebahatika kupata watoto 5 wa kike 3 na wa kiume 2. Kuhusu shughuli zangu binafsi Mimi ni mjasiriamali ambaye nimefanya shughuli mbali mbali na kubuni miradi mbali mbali, kwa mfano nimewahi kuanzisha kampuni ya Ujenzi, kiwanda kidogo cha chaki, kuendesha biashara ya mtandao kupitia Makampuni mbali mbali ya kigeni , biashara hizi nimeachana nazo. Sasa hivi najishughulisha na kutoa huduma ya Ushauri wa biashara. Huduma ambazo nazitoa ni; Kutoa ushauri wa biashara kwa Wafanyabiashara wadogo wa kati na wakubwa, Kuandaa michanganuuo kwa ajili ya kuomba mikopo benki na misaada kutoka kwa wafadhili, Kutoa mafunzo ya Ujasiriamali kwa wafanyabiashara, Kuandaa mifumo ya utunzaji wa mahesabu na kuweka mifumo ya Kompyuta kwenye utunzaji wa hesabu, Kuandaa katiba za vyama na nyaraka za uandikishaji wa makampuni, Kuandaa nyaraka za Tenda, Kutoa ushauri kwa SACCOS ili ziendeshwe kwa ufanisi, Kutoa ushauri kwa Asasi zisizo za kiserikali NGO ili ziweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi, Kutoa ushauri nasaha na semina kwa wanafunzi. Mimi ni mtunzi wa vitabu na nimetunga kitabu cha Ujasiriamali kinachopendwa sana, kiitwacho, Mbinu za biashara na maarifa ya kupata pesa na utajiri. Kitabu hiki nilikitunga baada ya lengo la kuwafikia wajasiriamali kwa nja ya semina kukwama ambapo nilikuwa nikitoa matangazo kwenye magazeti lakini watu hawafiki. Kitabu hicho kinalenga kumsaidia mtu yeyote ambaye anatafuta utajiri kwa kufanya biashara ndogondogo hadi kubwa. Pia kinatoa maarifa, mbinu na mikakati mbalimbali ya kupambana na umaskini, kinatoa elimu ya biashara na mbinu mbalimbali za namna ya kupata pesa kwa njia halali ili kukurahisishia safari yako ya kuelekea kwenye kutafuta na kupata utajiri. Kitabu hicho kina sehemu mbili, sehemu ya kwanza inaeleza kuhusu taratibu za kuanzisha biashara, sheria, utafiti wa masoko, utunzaji wa hesabu za biashara na utatuzi wa matatizo ya biashara. Sehemu ya pili inaelezea kuhusu mawazo na mbinu mbalimbali za biashara unazoweza kuzifanya na kupata faida na hivyo kutajirika. Kitabu hicho ni matokeo ya utafiti na uzoefu katika kazi za ukaguzi nilizozifanya kwa kuangalia matatizo ya uendeshaji wa biashara mbalimbali pamoja na ushauri nilioutoa kwa watu walioomba ushauri kutoka kwangu. Kitabu hicho kilichapishwa kwa mara ya kwanza na Business Printers mwezi March mwaka 2008 na mpaka sasa zimechapishwa nakala 4,000 na kuuza nakala 3,000 kwa muda wa miaka 3.Kitabu hicho kiapatikana kwa njia ya Posta au email katika mfumo wa PDF unaweza kunitumia Sh. 5000 kwa MPESA Kwenye simu namba 0755394701 kisha ukanitumia email yako nami nitakutumia kwenye email yako kama kiambatanisho. Mafanikio yangu ni pamoja na kupata wateja wengi waliopata ushauri wangu na kuufurahia. Pia niliweza kupata wateja wengi walionunua kitabu changu na kukifurahia. Baada ya kuchapisha kitabu nimehojiwa na vyombo mbali mbali vya habari kama vile; ITV, Star TV, TBC 1 TV na TBC1 Radio na Wapo Radio. Hata hivyo kila palipo na mafanikio hapakosi matatizo. Nimekuwa na malengo ya kuwa na kipindi changu cha Ujasiriamali ambacho kimekubalika na vyombo vya habari mbalimbali pamoja na wasikilizaji na watazamaji, lakini nimekosa wadhamimini wa kukidhamini kipindi hiki ambacho kinapendwa sana na wajasiriamali. Malengo yangu ya baadaye ni kuhakikisha kwamba elimu ya ujasiriamali inaenezwa nchini Tanzania. Pia kuendelea kutoa huduma bora za ushauri kwa Wafanyabiashara wadogo wa kati na wakubwa,kwa SACCOS na Asasi zisizo za kiserikali NGO ili ziweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi. Ili kutekeleza hayo nitafanya yafuatayo; Kutoa elimu kwa njia ya makala, Radio, Televisheni na semina na Video ya ujasiriamali. Ninao mpango wa kutunga vitabu zaidi katika masuala ya Ujasiriamali saikolojia na ushauri nasaha. Mimi ni mwana harakati wa kupigana vita na umasikini ambaye pia naamini kwamba umasikini hapa Tanzania utatoweka pale ambapo elimu ya ujasiriamali itakapokuwa imeenezwa kila sehemu, kwani watu wengi wanakosa fursa za kiuchumi au kujiingiza katika uwekezaji mbovu kwa kukosa maarifa. Pia naamini katika kutenda. Tatizo la Watanzania wengi ni kuwa na tabia ya kulalamika na kulaumu pale wanapokutana na mtatizo, lakini hawajitumi na wala hawatafuti maarifa na njia za kutatua matatizo. Nawashauri viongozi wa Serikali pamoja na wadau wengine waweke utaratibu wa kufundisha elimu ya jasiriamali kwa vijana wetu kuanzia Shule za msingi hadi elimu ya juu ili mara wamalizapo shule wawe waajiri kwa kuwa wajasiriamali badala ya kuwa waajiriwa. Pia nashauri Serikali kutilia mkazo elimu ya juu kwa watanzania ili kuwakomboa Watanzania. Nchi zilizokazania elimu kwa watu wake, kama vile India, Japan na China, wamejikuta wakiwainua watu wake ambao walipata ajira nje ya nchi na kuinua uchumi wan chi kwa ujumla. Eneo lingine ambalo ninaloliona kuwa linatakiwa kuangaliwa ni uwezeshaji wa wananchi kwa kupatiwa mitaji. Utaratibu unaoweza kutumika ni kutoa ruzuku si kutoa mikopo kwa wajasiriamali kwani wengi hawana uwezo au ujuzi wa kuizungusha mikopo hiyo na kurejesha. Mbinu nyingine inayoweza kusaidia kuwainua wananchi ni njia ya kuanzisha asasi za wananchi zitakazo wafundisha utaratibu wa kujiwekea akiba na kukopeshana mfano VIKOBA pamoja na SACCOS. Ninaishauri Serikali kuweka mkazo kwenye kilimo hasa cha Mashamba makubwa na kuanzisha viwanda vya kusindika mazao kuyaongezea thamani badala ya kuuza kama malighafi ambapo bei yake ni ndogo. Pia serikali iangalie kuweka utaratibu mzuri wa masoko ya mazao ya wakulima hasa wadogo wadogo ili kuondoa umasikini wa kipato kwani tatizo lao kubwa ni masoko ya kuuzia mazao yao. Wataalamu wa uchumi wameonyesha kwamba nchi zote zilizoweka mkazo kuwekeza katika kilimo uchumi wake uliinuka haraka sana na huwa hauyumbi yumbi. Ninatoa ushauri kwa wajasiriamali kwamba wakitaka kuanzisha biashara wasikurupuke wafanye utafiti kwanza kuhusu masoko na siri za biashara wanayotaka kuifanya.Wanaweza kufanya utafiti kwa kuwauliza watu waliofanikiwa katika biashara hizo au washauri wa biashara kama mwandishi wa makala za ujasiriamali na mshauri wa biashara. Kwa kuwa tatizo la watu wengi ni mtaji waanze kujenga tabia ya kujiwekea akiba kidogo kidogo na kufanya biashara ambazo zinaanza na mtaji kidogo halafu wapanue biashara kidogo kidogo. Mfano wa biashara ambayo wanaweza kuanza kwa mtaji kidogo ni ya Ufugaji wa kuku wa kienyeji na bustani. Kama wewe ni mjasiriamali mwerevu, ili ufanikiwe unapaswa kutafuta ushauri kutoka kwa wataalamu kwa ajili ya kutatua matatizo yako.

No comments:

Post a Comment