Sunday, November 25, 2012

JINSI YA KUTAMBUA HAIBA YAKO

Jinsi ya Kutambua Haiba Yako Katika utafiti wa kuchunguza athari za msongo wa mawazo katika moyo, madaktari Mayer friedman na Ray Roseman waliweza kuwaweka watu katika makundi ya haiba mbili; yaani haiba kundi A na haiba kundi B. Madaktari hawa waligundua kuwa hata kama kazi na aina ya maisha ingefanana, watu wa haiba kundi A wangekuwa na nafasi mara 3 kuteseka na msongo wa mawazo, magonjwa ya moyo, shinikizo la damu n.k. na watu hawa mara nyingi huwa wanamaudhi kwa jinsi wanavyojibu au kuongea na wengine, na hili limekuwa likiwaongezea msongo wa mawazo maradufu. Makundi haya yamewekwa ili kukuwezesha wewe kujua uko upande gani. Usichanganyikiwe wala kushtuka pale utakapojikuta una tabia za makundi yote mawili, mara nyingine inaamaanisha kuwa uko vizuri katika kuhakikisha mambo yanafanyika inavyotakiwa au unavyotaka yawe. Ila kama unajikuta una tabia zaidi ya nusu za haiba kundi A, inabidi uchukue uamuzi wa kutafuta kubadilika au kubadilisha mtazamo ulionao katika maisha, kabla haujajihatarishia maisha yako wewe mwenyewe. Haiba Aina ‘A’ Ni watu wa ushindani katika kila kitu wafanyacho. Watu wenye haiba ya kutumia nguvu na kulazimishisha . Hufanya mambo yao mengi kwa haraka. Huwa na uchu wa kupandishwa vyeo na kujulikana katika jamii. (Hata kama hawana sifa). Hutaka sana kujulikana na kuheshimiwa kwa kile walichokifanya. Hukasirishwa kwa haraka na watu au matukio fulani. Huongea mara kwa mara kwa kufoka au kwa vitisho. Hupenda kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Hutembea na hata kula kwa haraka. Mara nyingi kuchukizwa sana pale wanapocheleweshwa. Hujali sana muda na kukazana kumaliza mambo kwa muda uliopangwa (meeting deadlines). Kila mahali huwepo kwa wakati na kwa muda muafaka. Mara kwa mara misuli yao ya uso huonyesha, kumaanisha, kuogopesha au ukali. Haiba Aina ‘B’ Siyo watu wa ushindani mfano, makazini, michezoni, masomoni n.k. Ni watu walio rahisi, na huyakubali mazingira, hufanya vitu taratibu na kwa kufuata kanuni. Huendelea na kuchukuliana na hali ya kazi iliyopo. Huridhika na nafasi waliyonayo katika jamii. Hawahitaji kujulikana au kutambulika katika jamii au hata katika matukio. Siyo rahisi sana kuwaudhi. Mara nyingi hufurahia sana wanapokuwa peke yao. Ni wavumilivu. Hupendelea kufanya kitu kimoja kwa muda muafaka kabla ya kwenda kwenye kitu kingine. Hutembea, na kula kwa nafasi na utulivu. Hawakimbizwi sana na muda, siyo wakukimbizana sana na kumaliza kazi. Mara nyingi ni wachelewaji. Nyuso zao ni za kufurahi na siyo za mikunjo. KWANINI UKO VILE ULIVYO? Vyovyote haiba yako ilivyo na kwa vyovyote unavyowachukulia wenye tabia ngumu fahamu kuwa mfano huo ulishakuwepo miaka mingi iliyopita, labda zaidi ukiwa mtoto ndiyo ilikuwa chanzo cha vile ulivyo leo; Mwanasaikolojia mmoja aliuita mfumo huu...“A child is a father of a man” yaani mambo tunayoyaona au unayoyaona kwa mtoto hutupa picha halisi ya ukubwa wake utakavyokuwa. Zaidi ya asilimia sitini ya yote yanayoendelea maishani mwetu leo yanachangiwa na makuzi yetu tukiwa watoto. Wengi wetu tumejiharibia misingi yetu ya uwezo wa kuishi na watu wenye tabia ngumu na hivyo kujikuta tunaumizwa tokea tukiwa watoto wadogo. Habari njema ni kwamba hakuna ulazima wa kubaki vile ulivyo, mabadiliko yanawezakana, inawezekana katika hatua yoyote kubadili mtazamo au muonekano wako na kuboresha ujasiri wako. Tujaribu kuangalia baadhi ya sababu zinazosababisha mtu kujiona au kujitazama vibaya, hii itakuwezesha wewe kujua uko wapi na kwanini. Watu wa kwanza kabisa waliowahi kuwa karibu na wewe ni baba na mama yako au yeyote aliyechukua nafasi yao, mfano mlezi, babu, bibi nk. Kutokana na mtazamo wao juu yako, hapo wewe umetengeneza au kuzalisha mtazamo juu yako mwenyewe na jinsi unavyojithamini au kutojithamini. Kwa lugha rahisi ni kwamba, jinsi unavyojiangalia ulivyo leo kunatokana kwa kiasi kikubwa na jinsi wao walivyokuwa wanakutazama, kama walikuona wewe lofa na mjinga basi kuna uwezekano mkubwa na wewe leo utajiona lofa tu. Najua wapo wazazi wasio na hekima wala wema kwa watoto wao, huwasababishia watoto wao majeraha ya kimwili, kihisia na hata kiakili, uzuri ni kwamba fungu la wazazi hawa ni dogo. Ingawa inawezekana sana kwa wazazi au walezi au watu wazima wowote kusababisha majeraha na athari kwa watoto mara nyingine pasipo kujua kwamba wanafanya hivyo. Katika kuongea na wazazi lukuki nimegundua kwamba asilimia kubwa ya watoto wameharibiwa na wazazi wao wenyewe, pasipo wazazi kujua kuwa wanawaharibu watoto wao. Wazazi ambao huwalinda na kuwatetea sana watoto wao, wakijaribu kuwafanyia kila kitu kwa niaba ya watoto hao, kwa njia hii wazazi hawa hutengeneza watu wazima wenye utegemezi mkubwa, wasioweza kufanya kitu chochote wenyewe wala kusimama kwa miguu yao wenyewe. Unakuta hata kazi za shuleni mama ndiyo anafanya, mtoto anakuwa hata kuosha mwili wake hajui, na hawa ndiyo wale ambao ndoa huwashinda mapema. Wale wazazi au walezi ambao hutoa mahitaji kwa watoto wao lakini hushindwa kuonyesha kwa matendo upendo wao kwa watoto wao (mfano. Kuongea nao, kucheka nao, kucheza nao n.k.) hutengeneza kizazi kinachoamini kuwa hakipendeki, hakina mvuto, kisicho na thamani na kisichostahili kupendwa. Baba haijalishi unatoa mahitaji yote yanayohitajika nyumbani kwako, hilo siyo pekee watoto wako wanalolihitaji kutoka kwako, wape muda wakuwa pamoja nao, waruhusu kucheza na wewe kidogo, toka pamoja nao, jibu baadhi ya maswali yao, waruhusu kujua kumbe baba au mama anaweza kuwakaribu na sisi pia. Wazazi au walezi ambao kila mara humwekea mazingira mtoto kujiona aliyeshindwa, kila wakati ni wakufeli tu, wazazi hawa ni wale wanaosema kwa nini mtoto asijitahidi, kwanini asiwe wa kwanza darasani, ni mpumbavu n.k.. hali hii huharibu kabisa imani ya mtoto kwake yeye mwenyewe, huua kule kujiamini kwake na pia kutokiamini kile anachokifanya. Yawezekana kuna vitu vilivyoonekana katika makuzi ya mtoto ambavyo hakuna wa kulaumiwa lakini bado vitu hivi huathiri sana kujiamini na kujithamini kwa mtoto yule. Mtoto au watoto wanaohama hama au kuhamishwa shule mara kwa mara, kwa sababu zao binafsi au kwa sababu ya kuhama hama kwa wazazi hupata shida yakujiona wapweke kwa maana kila wakati hupata kazi ya kutengeneza marafiki wapya na kwa muda fulani hali hii huathiri haiba zao na kujenga kitu tunachokiita “inferiority complex” Tufanye nini?? Kitu cha kwanza ni kukubaliana na ukweli kwamba mtazamo wako (jinsi unavyojitazama) hubadilika badilika. Tena hubadilika kiasi ambacho mara nyingine huwezi kutambua. Unaweza kuchagua mwenyewe jinsi unavyotaka mtazamo wako uwe. Kwa mfano; Kufanikiwa au kushindwa Jaribu kutoangalia nyuma kule ulikowahi kushindwa zaidi, kila mtu ana historia ya kushindwa siyo wewe tu. Wacheza mpira maarufu duniani, mara nyingine hukosa magoli rahisi kabisa lakini hakuna hata mmoja aliyeacha kucheza au kuharibu fani yake kwa sababu ya kukosa goli. Wala hakuna aliyekiri kuwa yeye siyo bora kwa sababu tu ya kukosa goli moja. Ni vema kukumbuka kule tulikowahi kushindwa kama tu tunataka kujifunza katika makosa yetu, na siyo kwa kutaka kujisononesha na kujilaumu kwa namna tulivyokosea. Jifunze kuziacha historia za kufeli na kushindwa zifukiwe katika yaliyopita. Tengeneza mafanikio yako wewe mwenyewe anza katika hali ya chini kabisa, chagua vile vitu usivyo viweza kabisa kuvifanya mfano; Kuzungumza mbele ya watu, kuimba, kuogelea, kuwa kwenye usaili, kusimama mbele ya kamera n.k anza kuvifanya kwanza kupitia ufahamu wako (viwaze akilini) hali hii inaitwa (creative visualization) ni njia majawapo bora ya kufanya mazoezi ya vile tunavyoshindwa katika fikra zetu, kwanza jitahidi kujitazama fikrani ukiwa au ukifanya vitu hivyo kwa ushindi hadi ufahamu wako utakapoizoea hali hiyo na kuacha kutuma jumbe za kushtuka (kupanick) au uwoga wakati utakapokuwa unafanya vitu vile kihalisi. Katika kufanya mazoezi ya kufikiria kimtazamo, chagua kufanya katika utulivu mchana au jioni. Muda kabla hujaenda kulala ni mzuri zaidi. Rudia zoezi hili mara kwa mara mpaka uzoee na fikra zizoee. Andika vile vitu uvipendavyo juu yako mwenyewe, kama kuna mtu anayesema kuwa hana kitu cha kuandika basi mtu huyo hajafikiri kwa undani au ni mwongo, kila mtu ana kitu chema ndani yake. Kama ukishaandika vitu hivi, angalia tabia ya vile vitu ulivyoviandika pale, kama vitu hivyo vikifanywa na mtu baki usiyemjua je utasema yeye ni mtu mbaya? Kama siyo, kwa nini wewe unajiona usiyefaa na uliyejaa mabaya tu? Badala ya kutazama yale yaliyo mabaya na ya kushindwa katika historia yako tazama mafanikio yako. Kila mmoja ana mafanikio ya aina fulani, hata kama ni madogo kiasi gani. Hata kama unatazama yale yaliyowahi kufanyika huko awali basi yatazame katika mtazamo chanya. Wengi wetu hatuchukui muda kujiuliza vyanzo vya mitazamo yetu hasi, tunaamua kuikubali tu na kuikumbatia na kuifanya asili yetu. Ila mara tu utakapo gundua kuwa tatizo siyo lako wewe bali ni mazingira uliyokuziwa au aina ya wazazi uliokuwa nao basi utaacha kujidharau. Wako watoto wanaofurahia kupelekwa shule za bweni mbali na nyumbani, ila wako ambao hawapendi kabisa lakini wanalazimishwa, hali hii hupandikiza ndani ya watoto hawa upweke, hofu, msongo wa mawazo na kutokutulia (nazungumzia utulivu wa ndani) jambo ambalo huendelea hata katika utu uzima wao. Wako wengi ambao tabia zao za leo zilianza kuharibikia katika shule za bweni mbali na wazazi kwa mfano tabia za kusagana au kuingiliana kinyume na maumbile

No comments:

Post a Comment